MASHINDANO YA AFCON 2027 KUFANYIKA MKOANI ARUSHA- RC MAKALLA







 *_Amshukuru Rais Dkt. Samia kwa kutoa fedha Bilioni 340 kutekeleza ujenzi wa uwanja huo_* 

 *_Awahamasisha wananchi kuchangamkia fursa za Biashara, utalii, Mahoteli na usafirishaji_* 

 *_Aipongeza Taifa Stars kwa kufuzu hatua ya 16 bora kwenye Michuano ya AFCON 2025_* 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo  unaojengwa kwaajili ya kutumika kwenye michuano ya Soka kwa Mataifa ya Afrika AFCON-2027, akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kwa wakati fedha za kutekeleza ujenzi huo.

Mhe. Makalla ambaye amekagua ujenzi wa uwanja huo leo Jumatano Disemba 31, 2025 amesema kufikia leo ujenzi wa uwanja huo umefikia zaidi ya asilimia 70, akisema serikali pia katika Shilingi Bilioni 340 za kutekeleza mradi huo tayari zimelipwa zaidi ya Shilingi Bilioni 200 na hivyo kumfanya Mkandarasi kutoidai serikali kwa kazi alizozifanya mpaka hivi sasa.

"Serikali haidaiwi kwa kazi zilizofanyika mpaka sasa na hii inadhihirisha dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba yeye ameweka dhamira ya Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 na ndio maana amekuwa akisimamia kwa karibu na kutusukuma kuhakikisha Mkandarasi analipwa kwa wakati ili kazi ikamilike kwa wakati na kwa viwango vilevile vilivyokusudiwa." Amesema Mhe. Makalla.

Katika hatua nyingine Mhe. Makalla pia amewahamasisha wananchi wa Mkoa wa Arusha kuchangamkia fursa za biashara, utalii pamoja na utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo Mahoteli, vyakula na usafirishaji zitakazotokana na ujenzi wa uwanja huo na ujio wa michuano ya AFCON 2027, Akiipongeza pia Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kufanikiwa kufuzu kwenye hatua ya 16 bora kwenye Michuano ya AFCON inayoendelea huko nchini Morocco.

Post a Comment

Previous Post Next Post