MKURUGENZI wa Kitaifa wa Miss World Tanzania, Mustafa Hassanali amezinduzia Jukwaa la Kampuni ya 361 Degrees Africa linalolenga kuwatambua, kulea na kuwawezesha wasichana wa Kitanzania ili kuwakilisha taifa kwa heshima katika urembo wenye akili na dhamira njema
Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam ametoa wito kwa watu binafsi na waandaaji wa matukio wanaotaka kuendesha mashindano rasmi ya Miss World Tanzania kwa ngazi ya mkoa kuwasilisha maombi yao ili waweze kupata leseni zakuwawezesha kuendesha mashindano hayo katika maeneo yao husika
Aidha,amesema wamiliki wa leseni watakaoidhinishwa watapewa mamlaka ya kipekee kusimamia mashindano hayo katika mikoa yao ili kuhakikisha ushiriki unakuwa mpana kwa nchi nzima.
“Mashindano ya ngazi ya mikoa yatafanyika kupitia wamiliki wa leseni watakaorasimishwa nchini kote. Matukio haya yatachagua washiriki bora watakaopanda hatua hadi fainali za kitaifa jijini Dar es Salaam, hivyo kuhakikisha ujumuishwaji na fursa sawa kwa wasichana kutoka kila mkoa,” amesema
Sanjari na hayo mesema kupitia Jukwaa hili litaanzisha enzi mpya ya urembo wenye malengo katika kuwatambua na kuwalea wanawake vijana wenye uwezo wa kipekee wanaoonyesha umahiri, uongozi na falsafa ya kimataifa.
Sambamba na hayo,amesema Mshindi wa shindano la kitaifa atabeba taji la Miss World Tanzania na kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mashindano ya Miss World 2026 kama balozi wa urembo, utamaduni na dhamira ya ubinadamu.Katika hatua nyingine Hassanali amewahimiza wazazi na walezi kuwaunga mkono watoto wao wa kike ili waweze kushiriki katika jukwaa hilo ambalo amesema lina uwezo wa kuinua na kubadilisha maisha yao.


