Na mwandishi wetu
Dar es Salaam
MKUUwa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, amesema mabadiliko ya jina la Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) ni hatua ya kimkakati inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa na kufikia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mabadiliko ya jina la Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na kuzindua nembo mpya ya TNCC, Mheshimiwa Mpogolo alisema hatua hiyo inaakisi mageuzi ya kimfumo na kiuendeshaji yatakayoiwezesha TNCC kuwa taasisi imara, shindani na yenye sauti ya kuaminika kwa wafanyabiashara ndani na nje ya nchi. Alisisitiza kuwa sekta binafsi ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi, huku Serikali ya Awamu ya Sita ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara.
Kwa upande wake, Rais wa TNCC, Bw. Vicent Minja, alisema mabadiliko hayo yanafungua zama mpya za kuimarisha uwakilishi wa wafanyabiashara, kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana, pamoja na kukuza mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa Taifa.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TNCC, Bw. Oscar Kissanga, alisema mabadiliko ya jina na nembo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama na kuimarisha ushindani wa wafanyabiashara wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa uzinduzi rasmi wa nembo mpya ya TNCC, hatua inayofungua ukurasa mpya wa mwelekeo na uongozi wa chemba hiyo.

