UTT -AMIS YAFIKIA THAMANI TRILIONI 3.2 ONGEZEKO LA UKUAJI WA TRILIONI 1:MIGANGALA

 


Na mwandishi wetu

Dar es Salaam 

MKURUGENZI Mtendaji wa taasisi ya Uwekezaji wa pamoja( UTT-AMIS) ,Simon Migangala amesema mwaka 2024 mifuko ya UTT-AMIS ilikuwa na shilingi trilioni 2.2 lakini mwaka huu imeongezeka na kufikia zaidi ya shilingi trilioni 3.2 ongezeko la trilioni Moja linatokana na kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji pamoja na ongezeko la idadi ya wawekezaji

 Amesema zaidi ya wawekezaji 140000 wapya wameongezeka hadi kufikia wawekezaji 500000 ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa na mafanikio kwa mwaka huu.

Hayo yamebainishwa Leo Desemba 19,2025 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Migangala wakati wa mikutano ya mwaka 2025 kwa wawekezaji wa mifuko ya taasisi hiyo ambayo ni Umoja,Wekeza Maisha,Ukwasi,Kujikimu,Hatifungani na Watoto.

Amesema kwamba UTT AMIS inaendelea na jitihada za kuwawezesha wawekezaji ili waweze kuzifikia fursa za uwekezaji.

Ameeleza kuwa mfuko wa Umoja umefikia thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 400,huku ukiendelea kukua kwa faida ya asilimia 12.

Aidha, amesema UTT -AMIS inaendelea kutumia mbinu na njia mbalimbali za kisasa ili kuwawezesha wawekezaji na makundi yote kuwekeza katika mifuko hiyo kulingana na uwezo na malengo Yao ya kifedha.

Hata hivyo amesema taasisi hiyo imeahidi kuendelea kuchukua hatua za kuvutia wawekezaji wengi zaidi kwa kufungua ofisi kwa baadhi ya mikoa kama Morogoro na Kahama pamoja na kuimarisha elimu ya uwekezaji kwa umma ili kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTT-AMIS,Profesa Faustin Kamuzora amesema taasisi za uwekezaji katika sekta ya fedha zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi ,huku UTT -AMIS ikiendelea kujiimarisha pamoja na kuongeza thamani ya uwekezaji kwa watanzania

Aliendele kwamba UTT-AMIS Kwa Sasa ina mifuko Saba ya uwekezaji na imejipanga kuongeza tija ya mazao ya mifuko hiyo kwa lengo la kufanikisha faida kwa wawekezajii wake.

Aidha,amesema uwekezaji kupitia taasisi hiyo ni rahisi na unamuwezesha mwananchi wa kawaida kushiriki kikamilifu katika sekta ya fedha,ambapo mwekezaji huweka fedha zake na taasisi hufanya Kazi ya kuzisimamia na kuziwekeza kitaalamu kwa lengo la kuzalisha faida.

UTT-AMIS inaendelea kujikita katika eneo la usimamizi wa Mali(wealth management) ili kuhakikisha wawekezaji wananufaika ipasavyo kutokana na uwekezaji wao pamoja na kuimarisha Imani kwa umma katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja

Post a Comment

Previous Post Next Post