WADAU WA MAENDELEO NCHINI KUNUFAIKA NA MABORESHO MAPYA YA MAZINGIRA YA BIASHARA





Na mwandishi wetu

Dar es Salaam 

 WAFANYABIASHARA wawekezaji na wazalishaji kutoka sekta mbalimbali nchini wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja na maboresho mapya ya mazingira ya biashara yanayoandaliwa na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA). Maboresho haya yamechochewa na mazungumzo ya kimkakati yaliyofanyika kati ya Rais wa TCCIA, Bw. Vicent Minja, na mfanyabiashara mashuhuri nchini, Bw. Rostam Aziz.

Katika mazungumzo hayo, wadau hao wakubwa wameweka mbele maslahi ya wanachama wa TCCIA na wafanyabiashara kwa ujumla, wakisisitiza umuhimu wa kuwa na chemba imara ambayo inawatetea, inasikika na inaongoza katika mchakato wa kutengeneza sera rafiki za biashara.

Bw. Rostam Aziz alisisitiza kuwa uwepo wa Chemba madhubuti ni nguzo kuu ya mafanikio ya wafanyabiashara na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

“Chemba ni chombo kikubwa kwa ukuaji wa biashara. Inapaswa kupata sapoti kutoka kwa wafanyabiashara na hata kwa Rais wa nchi. Tukijenga Chemba imara, tunajenga Tanzania yenye uchumi madhubuti. Let’s start a new chapter — Chemba ichukue nafasi yake katika taifa,” alisema.

Akiendelea, Rostam alitoa wito kwa Watanzania kutambua mchango wa wafanyabiashara wazawa katika kuimarisha uchumi.

“Mimi nilipopitia changamoto, Chemba ilinilinda. Wafanyabiashara wakiona jinsi Chemba inavyotetea maslahi yao, wataelewa umuhimu wake. Ni wakati Watanzania waunge mkono juhudi za wafanyabiashara wazawa badala ya kuwanyooshea vidole,” aliongeza.

Kwa upande wake, Rais wa TCCIA, Bw. Vicent Minja, alibainisha kwamba mafanikio ya chemba hayatenganishwi na mafanikio ya wanachama wake.

“Chemba ikifanya vizuri, kila mfanyabiashara atanufaika. Tunahitaji kuiimarisha upya, kuipa nguvu na kuhakikisha sauti yetu inasikika kwenye majukwaa ya kutengeneza sera. Tukisimama kama mtu mmoja kupitia Chemba, changamoto za kibiashara zitashughulikiwa kwa ufanisi zaidi,” alisema Minja.

Mazungumzo haya yametoa dira mpya ya ushirikiano kati ya TCCIA na wadau wakubwa wa sekta binafsi nchini, yakilenga kuijenga chemba jumuishi, yenye nguvu na inayoweza kuongoza mageuzi chanya katika mfumo wa biashara na uwekezaji nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post