WAKRISTO NI WAJIBU WAO KUISHI KWA AMANI SIO CONDITION:MHASHAMU ASKOFU DKT.CHILONGANI

Na mwandishi wetu

DODOMA

ASKOFU wa Kanisa Anglikana Tanzania ,Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) Dkt. Dickson Chilongani, amewataka Watanzania kuitunza na kuilinda amani ya taifa kwa kumtanguliza Mungu.

Pia amewakumbusha Wakristo kuwa wao ni mfano wa kuishi kwa amani, akirejea maandiko ya Biblia yanayomtaja Yesu Kristo kama Mfalme wa amani na kuhimiza waumini kutafuta amani na utakatifu, kwani vitu hivyo viwili vinakwenda pamoja.

Aidha amesisitiza kuwa jukumu la viongozi wa dini siyo kuhukumu au kulaumu pande zinazokinzana, bali kuhubiri habari njema ya wokovu na kuhimiza amani, maombi na mazungumzo ya kujenga taifa.

Akitoa ujumbe wa Krismasi,jana katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Dodoma,Askofu Chilongani alisema maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania yamefanyika katika mazingira tofauti na ilivyokuwa mwaka 1961, wakati Hayati Mwalimu Julius Nyerere alipotangaza uhuru wa Tanganyika kwa shangwe na furaha kubwa, wananchi wakijaa matumaini na mshikamano.

Alikumbusha kuwa tarehe 9 Desemba 1961, Watanzania waliipokea habari ya uhuru kwa vifijo, nyimbo na maandamano ya amani, wakibeba bendera za TANU na matawi ya miti kuashiria ushindi na mwanzo mpya wa taifa huru, hali ambayo alisema ni kinyume na mazingira ya sasa yaliyojaa hofu ya maandamano, vurugu na matumizi ya nguvu.

Akitaja mifano ya kibiblia, aliwahimiza waumini kuangalia simulizi la Daudi na Abisalomu, pamoja na kuzaliwa kwa Yesu Kristo kama kielelezo cha Mungu kuingilia kati historia ya mwanadamu kwa lengo la kuleta wokovu wa milele kwa watu wote.

Askofu Chilongani alisema matukio ya hivi karibuni yameibua hofu miongoni mwa wananchi, ambapo baadhi ya majiji yalionekana kuwa matupu, shughuli za kijamii na kiuchumi zikisimama, huku milio ya mabomu ya machozi na risasi ikitawala.

Alisema hali ambayo haijawahi kushuhudiwa kwa kiwango kikubwa hapo awali.

Alisema imefika hatua raia kuwaogopa askari na askari kuwaogopa raia, jambo linaloashiria kupungua kwa imani na mshikamano wa kijamii, na kusisitiza kuwa suluhisho la hali hiyo ni taifa kumrudia Mungu na kumpa nafasi ya kutawala mioyo ya watu wote.

Hata hivyo, Askofu Chilongani alisisitiza kuwa jukumu la viongozi wa dini siyo kuhukumu au kulaumu pande zinazokinzana, bali kuhubiri habari njema ya wokovu na kuhimiza amani, maombi na mazungumzo ya kujenga taifa.

Askofu Chilongani aliwakumbusha Wakristo kuwa wao ni mfano wa kuishi kwa amani, akirejea maandiko ya Biblia yanayomtaja Yesu Kristo kama Mfalme wa amani na kuhimiza waumini kutafuta amani na utakatifu, kwani vitu hivyo viwili vinakwenda pamoja.

“Amani ya kweli haitokani na nguvu wala vitisho, bali inatokana na kumwamini Yesu Kristo, maombi, mazungumzo na matendo mema,” alisema Askofu Chilongani.


Post a Comment

Previous Post Next Post