MASHAURI NA MLEZI WA BODABODA NA MAMA LISHE AMUOMBA WAZIRI MKUU NCHEMBA KUUCHA LEGACY YA KUINUA MAKUNDI YA KIUCHUMI

 

MLEZI na mshauri wa makundi ya Maafisa Usafirishaji maarufu kama bodaboda, wamachinga na mama lishe, Ndugu Shaban Omary Matwebe, amemuomba Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Nchemba, kuacha alama ya kudumu (legacy) kwa kuwasaidia makundi hayo matatu kuvuka changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.

Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu Matwebe amesema makundi ya bodaboda, wamachinga na mama lishe ni nguzo muhimu ya uchumi wa wananchi wa kipato cha chini, hivyo yanahitaji mikakati maalum ya kuwawezesha kiuchumi na kijamii. Amebainisha kuwa changamoto kubwa zinazowakabili ni pamoja na ukosefu wa mitaji, kukosa mifumo rasmi ya kifedha, pamoja na kutokuwa na sauti ya pamoja ya kuwasilisha kero zao serikalini.

Katika maombi yake, Matwebe ameshauri serikali, kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, kuanzisha mifuko maalum ya maendeleo kwa makundi hayo, ikiwemo kuwaanzishia vyama vya ushirika (SACCOS) vitakavyowawezesha kupata mikopo nafuu na kukuza shughuli zao kiuchumi.

Aidha, amependekeza kuundwa kwa tume maalum isiyozidi watu kumi itakayopita mikoani kote nchini, kukutana na kusikiliza kero, maoni na mapendekezo ya bodaboda, wamachinga na mama lishe, kisha kuandaa mrejesho rasmi utakaowasilishwa kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya hatua zaidi.

“Makundi haya yana mchango mkubwa katika ajira na ustawi wa familia nyingi. Ni wakati sasa wa kuyatambua rasmi na kuyawekea mifumo itakayoyawezesha kufanya kazi zao kwa usalama, heshima na tija,” amesema Matwebe.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo utasaidia kupunguza migogoro, kuongeza mapato ya wananchi na kuimarisha uchumi wa taifa kwa ujumla, huku ukimuacha Waziri Mkuu akikumbukwa kwa kuleta mageuzi chanya kwa sekta ya wananchi wa chini.

Post a Comment

Previous Post Next Post