Na Mwandishi wetu
Zanzibar
MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Hamida Mussa Khamis Shuduma, amevutiwa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), akieleza kufurahishwa kwake na huduma ya Certificate of Origin na umuhimu wake katika kukuza biashara na uchumi wa wananchi.
Mhe. Hamida ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea banda la TNCC lililopo katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar (Zanzibar International Trade Fair – ZITF), ambapo amesema huduma hiyo ni nyenzo muhimu kwa wafanyabiashara, hususan katika kurahisisha biashara za kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya TNCC, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa taasisi hiyo, Bw. Matina Nkurlu, amesema: “TNCC inaendelea kujikita katika kuwahudumia wafanyabiashara kwa kutoa huduma zenye tija, ikiwemo Certificate of Origin, ambayo ni chachu ya kufungua masoko ya kimataifa na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.”
Aidha, Mhe. Hamida amependekeza wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja kuhamasishwa kuipata huduma hiyo kupitia mabaraza ya biashara, ili kuongeza uelewa na kunufaika kikamilifu na fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.


