Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
TAMASHA la kimataifa la Sauti za Busara 2026 linatarajiwa kufanyika kuanzia Februari 5 hadi Februari 8, 2026, likitanguliwa na ufunguzi wa awali (soft opening) utakaofanyika Februari 4, katika eneo jipya la Viwanja vya Mnazi Mmoja, Stone Town, Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mapema leo Januari 20, 2026, Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Journey Ramadhan, alisema mwitikio wa tamasha la mwaka huu umekuwa wa kipekee, hali inayotokana na mchanganyiko wa eneo jipya, uwepo wa wasanii wakubwa pamoja na kuongezeka kwa mvuto wa kimataifa.
Ramadhan alisema ushirikiano kati ya waandaaji wa tamasha hilo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umewezesha kupanuliwa kwa tamasha hilo kwa kuzingatia masuala ya usalama na ustawi wa washiriki wote.
Alisema hamasa ya Tamasha la Sauti za Busara imezidi kupamba moto Zanzibar na maeneo mengine, huku maandalizi ya mwisho yakiendelea kwa kasi kuelekea tamasha hilo kubwa la kimataifa linalotambulika kama “Tamasha Rafiki Zaidi Duniani”.
Kwa upande wake, Afisa Programu wa Busara Promotions, Zakialulu Mdemu, alisema tamasha hilo limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kufikisha ujumbe wa kijamii kwa maelfu ya wananchi, ikiwemo kuhamasisha uelewa kuhusu Vituo vya Huduma za Kijinsia vya One-Stop pamoja na huduma nyingine muhimu zinazotolewa kwa jamii.
Mdemu alisema pia kumekuwepo na mwitikio mkubwa kwa mpango wa Gender@Work Tanzania, uliopokea jumla ya maombi 179 kutoka nchi 11, mpango unaolenga kuwawezesha wanawake katika nyanja za kiufundi na kitaaluma ndani ya tasnia ya muziki na matukio.
Aliongeza kuwa kupitia mpango wa Amplifying Women’s Voices, wanawake 30 tayari wamepatiwa mafunzo, ambapo wengi wao sasa ni wataalamu wanaofanya kazi kikamilifu katika sekta hiyo.
Aidha, alisema Tamasha la Sauti za Busara 2026 linaahidi siku nne za burudani ya muziki wa kiwango cha juu, mwingiliano wa tamaduni mbalimbali pamoja na mchango chanya wa kijamii, zitakazofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Stone Town.
Waandaaji wa tamasha hilo wamewahimiza wadau na mashabiki wa muziki kujihakikishia tiketi mapema, kutokana na mahitaji makubwa yanayoendelea kuonekana kuelekea kufanyika kwa tamasha hilo.
