CUF YATOA MSIMAMO KUPINGA MAAMUZI YA MSAJILlK WA VYAMA VYA SIASA KUTENGUA MATOKEO YA UCHAGUZI WA 2022

 

Na Mwandishi wetu

DAR ES SALAAM 

 CHAMA cha Wananchi (CUF)kimetoa msimamo wake na kupinga vikali maamuzi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ya kutengua matokeo ya uchaguzi wa viongozi wakuu wa kitaifa uliofanyika mwaka 2022, kikisisitiza kuwa maamuzi hayo hayana msingi wa kisheria na yamekiuka taratibu za ndani ya chama pamoja na misingi ya haki ya asili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 17,2026 jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa CUF Magdalena Sakaya amesema chama kilifanya mkutano mkuu wa uchaguzi mwezi Desemba 2021 kwa kuzingatia katiba na kanuni zake, huku Msajili wa Vyama vya Siasa akishiriki katika hatua zote kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchakato huo na kuthibitisha kuwa uchaguzi ulikuwa huru, wazi na wa haki.

“Kutokana na ushindani mkubwa wa wagombea katika nafasi za juu, Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa liliamua kutumia mamlaka yake ya kikatiba kutengua baadhi ya kanuni tatu ili kuruhusu wagombea wote kushiriki kikamilifu bila kuchujwa, hatua iliyolenga kuimarisha mshikamano na demokrasia ya ndani ya chama”,amesema na kusisitiza kuwa,

Katika uchaguzi huo, mkutano mkuu ulimchagua Ibrahim Haruna Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Taifa, Othman Dunga kuwa Makamu Mwenyekiti Bara na Mbarouk Size kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar, pamoja na kuchagua wajumbe wa Baraza Kuu kutoka kanda tisa kama inavyoelekezwa na katiba ya chama

Sakaya amesema baada ya uchaguzi huo, baadhi ya wanachama waliwasilisha malalamiko kwa Msajili wakidai kuwa washindi hawakupata zaidi ya nusu ya kura halali, lakini malalamiko hayo hayakufanyiwa maamuzi kwa muda mrefu hadi Februari 2026, ambapo ghafla Msajili alitangaza kuyabatilisha matokeo.

Amesema Chama kimehoji sababu ya maamuzi hayo kuchelewa kwa miaka kadhaa, kikieleza kuwa yanaonekana kuja katika mazingira ya kisiasa yaliyojaa mvutano, hususan baada ya uchaguzi mkuu wa 2025 na matamko ya CUF kuhusu masuala ya haki za binadamu na demokrasia nchini.

Kwa mujibu wa uongozi wa CUF, Msajili mwenyewe alikiri kuwa Baraza Kuu lina mamlaka ya kutunga na kutengua kanuni zake, lakini cha kushangaza alitumia hoja hiyo hiyo kuingilia mchakato wa ndani wa chama kwa kutaka kusimamia uchaguzi wa marudio, jambo ambalo chama kinasema ni nje ya mipaka ya mamlaka yake kisheria.

Aidha, chama kimeeleza kuwa Msajili alikiuka kanuni ya haki ya asili kwa kushindwa kuwapa fursa ya kusikilizwa viongozi waliotenguliwa kabla ya kutoa uamuzi dhidi yao, hali inayokiuka misingi ya katiba ya nchi na utawala wa sheria.

CUF imesema itachukua hatua zote za kisheria kulinda uhuru na mamlaka ya chama, ikisisitiza kuwa uchaguzi wa viongozi ni suala la ndani ya chama na haupaswi kuamuliwa na chombo kingine, huku ikiendelea kuwataka wanachama na Watanzania kwa ujumla kuendeleza mshikamano, amani na heshima kwa misingi ya demokrasia.

Katika hali isiyotarajiwa ghafla wakati mkutano wa kaimu katibu mkuu na waandishi wa habari ukiendelea kulitokea kundi lingine la wanachama wa chama hicho wakimpongeza msajili wa vyama vya siasa kwa maamuzi ya kutengua matokeo ya uchaguzi wa viongozi wakuu wa kitaifa, hali iliyopelekea jeshi la polisi kuweza kuingilia kati ili kusije kukatokea fujo na kuzua taharuki.

Mpaka habari inaandaliwa makundi yote mawili yalikuwa bado kwenye ofisi ya chama huku jeshi la polisi likiendelea kulinda amani na usalama katika eneo hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post