SERIKALI imetangaza hatua ya kihistoria inayoweza kubadili sura ya tasnia ya maudhui ya kidijitali nchini. Kupitia tamko lililotolewa katika Mkutano wa Mwaka wa Watoa Huduma za Utangazaji (ABC 2026) jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, amesema ada ya leseni kwa watoa maudhui mtandaoni imeshushwa kutoka Sh500,000 hadi Sh50,000, huku ada ya maombi ikiwa Sh10,000 pekee.
Ni punguzo la zaidi ya asilimia 90, hatua ambayo wengi wameitafsiri kama mlango mpya kwa vijana wabunifu, wanablogu na watengeneza maudhui waliokuwa wakikwama kwa gharama.
Hatua hiyo imekuja baada ya mazungumzo ya karibu mwaka mzima kati ya Tanzania Bloggers Network (TBN) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), yakilenga kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikizuia ukuaji wa sekta hii.
Zaidi ya hayo, ada ya wakusanyaji wa maudhui (Online Content Aggregators) imeshuka kutoka Sh1,000,000 hadi Sh100,000.
Aidha, kundi jipya la “Amateur” limeanzishwa mahsusi kwa vijana wanaochipukia, likiwawezesha kujisajili rasmi bila mzigo wa kifedha.
Kwa muktadha wa uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi, uamuzi huu unaweza kuwa kichocheo kikubwa cha ajira, ubunifu na mapato ya kodi kwa taifa, kama yalivyo maono ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
