Na Mwandishi Wetu
ZAIDI ya wafanyakazi na wananchi 2,000 kutoka Mkoa wa Njombe na maeneo mbalimbali nchini wamepatiwa huduma ya afya kupitia Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ambayo imeandaliwa na Wakala kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Mfuko .
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda wakati wa kufunga maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Mji Mwema mkoani hapa, ambapo amesema maadhimisho ya mwaka huu yamepata mwitikio mkubwa kwa taasisi na kampuni 150 kushiriki kutoka 70 za mwaka jana mkoani Singida.
Mwenda amesema pia maadhimisho hayo yameshuhudia umati wa wananchi ambao walikuwa wanatembelea mabanda na kujifunza mambo mbalimbali.
Amesema wananchi wamepata huduma za afya kutoka kwa madaktari bingwa wa OSHA, Hospitali ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Afya ya Akilli Mirembe na nyingine nyingi.
"Maadhimisho haya yametia fora kuanzia washiriki na huduma, kwani hadi leo tumetoa huduma ya afya kwa wananchi zaidi 2,000, pia tumetoa elimu ya ushauri wa kisaikolojia na mengine mengi, alisema.
Alisema pia OSHA kwa kushirikiana na washiriki wametoa vifaa mbalimbali kwa waendesha pikipiki, mama lishe na makundi mengine.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafangakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amewataka wafanyakazi kutoa taarifa iwapo wataona ofisi zao hazina tangazo la OSHA.
Nyamhokya alisema waajiri kujisajili kwa OSHA ndiko kunasaidia viongozi wa shirikisho hilo ambao ni watetezi wa wafanyakazi kuamini kuwa watumishi wanafanya kazi katika mazingira salama.
"Kama ofisini kwako huoni bango la OSHA toa taarifa TUCTA ili tuweze kuchukua hatua," alisema.
Alisema TUCTA imekuwa ikishirikiana na OSHA, ili kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira mazuri na wameona matokeo chanya kwa miaka kumi ya uongozi wake.
Rais huyo amesema TUCTA itaendelea kushirikiana na OSHA ili kuhakikisha sekta ajira inakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu amesema OSHA ni taasisi muhimu kwenye uchumi wa nchi na afya za wafanyakazi hivyo wataiunga mkono ili kufanikisha malengo yao.
Sangu amesema Rais Samia aliikuta OSHA ikiwa na magari 15 ambayo yalikuwa hayana uwezo wa kutoa huduma vizuri, ila kwa sasa wana zaidi ya magari 60 na wamenunua vifaa vya ukaguzi vyenye thamani ya shilingi bilioni 7.
Kwa mwingine Waziri Sangu ametoa miezi mitatu kwa OSHA, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Hifadhi na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kusajili na kukusanya madeni kwa waajiri wanaokiuka sheria inayosimia taasisi hizo.
Amesema waajiri wengi hawajajisali OSHA na WCF, huku kwa upande wa NSSF michango ikiwa ya kusuasua jambo ambalo halivumiliki kwa kuwa ni uvunjifu wa sheria.
"Natoa siku 90 yaani miezi mitatu kwa OSHA, WCF na NSSF muongeze kasi ya usajili wa waajiri na kukusanya madeni, kwani hali kwa sasa sio nzuri," amesema.
Waziri Sangu alisema takwimu zinaonesha kuna waajiri laki mbili ila waliosajiliwa OSHA na WCF hawafiki laki moja, hivyo hao laki moja waliobaki wanapaswa kusajiliwa kwa miezi mitatu ijayo.
Amesema miezi mitatu iliyopita alitoa maagizo kwa OSHA kusajili waajiri ambapo hadi jana taarifa zinaonesha zaidi ya waajiri 4,000 wameajiriwa, hivyo kuanzia mwezi ujao kazi iendelee na wale wanaokiuka hatua za kisheria zichukuliwe.
Sangu amesema NSSF ilikuwa inadai michango zaidi ya shilingi bilioni 300 kwa waajiri, ila kwa miezi tisa imeweza kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 270 sawa na asilimia 70 hivyo iongeze juhudi kukusanya na kuwachukulia hatua waajiri wazembe




