Na mwandishi wetu
Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama pia wananchi linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuzuia vitendo vya kihalifu kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji.
Akizungumza na waandishi wa habari Leo Desemba 22,2025 Jijini Dar es Salaam,SACP Muliro J.Muliro amesema hali ya usalama kwa ujumla ni nzuri na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida pamoja na mambo mengine yaliyotokea mwezi Octoba hadi Novemba 2025 .
Aidha , Jeshi la Polisi kwenye sehemu ya mashauri yaliyofikishwa ofisi ya Mashitaka na baadae Mahakamani kumekuwa na mafanikio yaliyowezesha baadhi ya watuhumiwa kupatikana na hatia hasa wenye makosa yanayohusiana na ukatili kwa wanawake na watoto.
Baadhi ya watuhumiwa waliopatikana na hatia ni Abubakari Memba @abuu Mkazi wa Mbagala alihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa kosa la kulawiti
Huku Julius Jasto @mbwambo mkazi wa Ukonga alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Ilala kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti
Watuhumiwa wengine ni Paul Elisha mkazi wa Kawe alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya Kinondoni kifungo cha maisha jela kwa kosa la kubaka na Erick Muhagama mkazi wa Kimara alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya Ubungo kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti.
Pamoja na Khalifani Ramadhani Mkazi wa Kiponza Chamazi alihukumiwa na Mahakama ya Temeka kifungo cha Miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na Jackson Tumwesige na Abrahamani Hassani @Mkwawa wakazi wa Ukonga walihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Ilala kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali.
Hata hivyo SACP Muliro J.Muliro alisema katika kueleka sherehe za Krismas na mwaka mpya, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam litaendelea kushirikisha na umma katika kubaini, kuzuia na kutanzua mambo ya uhalifu na kushirikiana na nyumba za ibada ili kuhakikisha usalama unaimarika kabla, wakati na baada ya ibada mbalimbali.
Pia Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wazazi na walezi kuwa na uangalizi wa karibu kwa watoto wakati wa matembezi na mikusanyiko mbalimbali, pia nyumba na makazi yasiachwe bila uangalizi kipindi chote.
Hata hivyo ameeleza suala la Usalama barabarani ukaguzi wa kushitukiza na kuwapima madereva wa vyombo vya moto umeanza. Polisi inatoa wito kwa watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria ili kuepusha ajali.
Alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali na za haraka za kisheria kwa wote watakao bainika kutenda makosa.
Aliendelea kwamba Polisi inawaonya na kutoa tahadhari kwa watu wenye tabia ya kupiga baruti au fataki bila vibali vya kisheria na kusababisha usumbufu na hofu kwa umma. Polisi haitasita kuchuka hatua kwa mtu yeyote atakaye kiuka sheria
