UTEKELEZAJI MRADI WA ‘BOLD’ WAVUTIA WADAU SEKTA KILIMO







Na Mwandishi Wetu, Arusha

WADAU mbalimbali wa maendeleo katika sekta ya kilimo nchini wameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ‘Biodiversity for Opportunities, Livelihoods and Development’ (BOLD), unaolenga kuinua sekta ya mbegu kwenye nchi zaidi ya 50 duniani ikiwemo Tanzania, kupitia tafiti zinazoendelea kufanyika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti pembezoni mwa warsha inayoendelea ya wadau wa mnyororo wa thamani wa rasilimali za vinasaba vya mimea inayofanyika kwenye Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable Center)  jijini hapa, wameelezea kufurahishwa na utekelezaji wa mradi huo.

Mratibu wa mradi huo kutoka  Global Crop Diversity Trust (Crop Trust),  Benjamin Kilian amesema mradi huo utakuwa mkombozi kwa wakulima wadogo, kwani  umebeba malengo saba  yatakayo leta matokeo endelevu kwenye tafiti za mbegu sambamba na kuongeza uzalishaji na uchakataji wa mazao yaliyosahaulika.

Aliongeza kuwa siku tano, watashiriki pia katika vikao vya ushirikiano, mijadala ya sera, na ziara za shambani ili  suluhisho za pamoja  zinazoweza kutekelezeka kwa mifumo ya chakula imara na jumuishi.

Aidha, Kilian aliipongeza Taasisi ya WorldVeg kwa kuwakutanisha pamoja wadau katika sekta ya  kilimo, na kubainisha kuwa  wamekuwa wakisaidia benki za kitaifa za vinasaba duniani kote, na Tanzania ni miongoni mwa washirika wao wakubwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Taifa  cha Hifadhi ya  Nasaba za Mimea  kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Dk. Mujuni Sospeter Kabululu amesema  kwa upande wa Tanzania,  wanashiriki katika  vifurushi vitatu vya kazi  kati ya vile saba, kwa kuangalia jinsi watakavyoimarisha mifumo  ya mbegu, mifumo ya uhifadhi katika mazao manne  ambayo ni ulezi, njugumawe, viazi vitamu na moringa.

“ Mazao haya yalichaguliwa kupitia  kikao cha wadau tulichokaa kuchagua ni aina gani ya mazao yaingizwe kwa ajili ya kuyafanyia tafiti pamoja na kuongeza matumizi yake,” amesema Dk Kabululu.

Naye Mkurugenzi Mkaazi wa  WorldVeg, Colleta Ndunguru amesema  wamekuwa na wasaa mzuri  kwani mradi huo umeweza kuwaweka pamoja  wataalamu zaidi ya 40  kujadili namna bora ya kuhifadhi nasaba za mimea pamoja na kuhifadhi mbegu za asili sambambana  kubadilishana uzoefu utakaochangia kukuza sekta ya mbegu duniani.

 “Tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na   wadau  wetu ambao ni Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) pamoja na  Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) katika kubadilishana  uzoefu na ujuzi   utakao tusaidia  kuzalisha mbegu zinazohimili magonjwa pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi,” alisema Ndunguru.

Naye Dk Adolf Saria  kutoka TOSCI,  amesema  mradi huo utasaidia kuhakikisha mbegu ambazo zimesahaulika zinapata nafasi.

Post a Comment

Previous Post Next Post