WAMACHINGA,BODABODA NA BAJAJI KUKUTANA JANUARI 2026 KUJADILI CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI

 


Na mwandishi wetu

DAR ES SALAAM 

MWENYEKITI wa  Shirikisho la Bajaji na Bodaboda Taifa,Said Chunja amesema wanatarajiwa  kuandaa kongamano kubwa la kitaifa litakalofanyika Mwezi Januari 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 28,2025 Jijini Dar es Salaam amesema kongamano hilo litafanyika kwa kushirikiana na Chama Cha wamachinga Tanzania na litawakutanisha wadau mbalimbali na lengo ni kusikiliza,kujadili na kutatua  changamoto za wamachinga na bodaboda nchini

Aidha ,amesema kongamano hilo halitawakutanisha wao  bali litawakutanisha pia viongozi wakuu wa serikali kwa lengo la kuwasilisha changamoto zinazowakabili maafisa usafirishaji(bodaboda), bajaji na wamachinga nchini.

"  Kwenye kongamano Hilo kubwa hatutakuwa sisi peke yetu tu,tutakuwa na kiongozi mkubwa wa serikali kumueleza changamoto zetu zinazotukabili wamachinga,boda boda na bajaji,"alisema Chunja

Naye Mwenyekiti wa Wamachinga Taifa,Ernest Matondo aliwashukuru wamachinga ,mama lishe kwa kuonesha uzalendo na nidhamu kwa kutoshiriki maandamano yaliyokuwa yamepagwa  kufanyika Desemba 9 na 25.

"Nawashukuru wamachinga na mama lishe kutii wito wa amani na kutoshiriki maandamano ,wameonesha  uzalendo,mshikamano na upendo ",

Pia ameiomba serikali kuwatafutia ajira rasmi mgambo wanaodaiwa kuwasumbua ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima mitaani

Hata hivyo alieleza changamoto zinazowakabili wafanya biashara wadogo na waendesha vyombo vya usafiri zipatiwe ufumbuzi wa haraka katika maeneo yote ya nchi.

Mwenyekiti huyo alisema kwamba waendesha boda boda wanakosa mikopo kwa wakati hali inayokwamisha juhudi zao za kujiendeleza kiuchumi.

"Tunaomba taasisi za kifedha na serikali kuwafikia ili waweze kujikwamua kiuchumi",alisema

Katika changamoto nyingine ameeleza kwamba bodaboda hukaa muda mrefu juani wakisubiri wateja ,hivyo tuaiomba serikali itengeneze miundombinu rafiki kama maeneo ya kupumzikia na kujistiri wakati wa kusubiri huduma.

Alitaja changamoto ya fursa za kifedha ambapo alieleza kuwa tayari Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo ya vijana,wanawake na makundi  maalum huku akiomba fedha hizo ziwafikie walengwa kwa wakati na kwa uwazi.

Post a Comment

Previous Post Next Post