- Aitaka Mahakama imzuie kupotosha umma kuhusu kesi
NaMwandishi wetu,
Dar es Salaam
Mwenyekiti wa MECIRA, Habibu Mchange, amesisitiza kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, anamtumia Tundu Lissu kama nyenzo ya kujinufaisha kisiasa na kifedha, huku akipotosha umma kuhusu mwenendo wa kesi inayomkabili Lissu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mchange alidai kuwa kauli na matendo ya Heche ikiwemo kutumia viunga vya Mahakama kuzungumzia shauri linaloendelea ni jaribio la wazi la kuingilia uhuru wa Mahakama na kuathiri mchakato wa haki.
Jana Heche alikanusha taarifa zilizoibuliwa na Mchange hivi karibuni kuwa Heche na wanaharakati waliojificha nje ya nchi wanaoongozwa na Maria Sarungi wanafanya kila wanaloweza kuhakikisha Lissu hawi huru kwani kwa kufanya hivyo wananufaika
Mchange ameeleza kuwa alichokifanya Heche jana ni kuichonganisha familia ya Lissu, Lissu mwenyewe na Mahakama na kwamba maneno yake yanataka kuionyesha Dunia kuwa mwenyekiti wake hatendewi haki huku akijua kuwa anaongea maneno hayo kimkakati
“Mahakama si jukwaa la siasa, kesi inapokuwa Mahakamani, viongozi wanapaswa kuheshimu mipaka ya kisheria, kauli za kisiasa kwenye viunga vya Mahakama ni upotoshaji wa umma na ni shinikizo kwa mhimili huru wa dola,” alisema Mchange.
Mchange alidai zaidi kuwa kuna mkakati unaoendeshwa na Heche pamoja na baadhi ya wanaharakati akiwemo Maria Sarungi, kuhakikisha Lissu haachiwi huru kwa wakati, kwa sababu kuendelea kwa kesi hiyo kunawanufaisha kupitia michango, kampeni na ufadhili kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi.
“Kuna watu hawataki Lissu awe huru, kesi yake imegeuzwa mradi, Kadri anavyoendelea kuwa mahabusu, ndivyo wanavyoendelea kuvuna kisiasa na kifedha,” alidai.
Kwa mujibu wa Mchange, hali hiyo imewafikia hata waliokaribu zaidi na Lissu, akisema familia ya Lissu haifurahishwi na namna ndugu yao anavyodaiwa kutumiwa kwa maslahi ya wengine.
Alidai kuwa ndicho chanzo kilichosababisha familia hiyo kuchukua hatua za kufikisha malalamiko polisi, baada ya kudai kuona michango iliyokusanywa kwa jina la Lissu ikipotea au kuibiwa.
“Familia iliona ndugu yao anageuzwa mradi. Ndiyo maana wakaamua kufika polisi walipoona michango ya Lissu inachukuliwa na watu wengine kwa maslahi yao,” alidai Mchange.
Ameongeza kuwa dada wa Lissu ameweka wazi msimamo wa kifamilia kwa kuomba kaka yake aachiwe huru, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu kama sehemu ya maridhiano, utu na kutuliza mvutano wa kisiasa.
Kwa mujibu wa Mchange, ombi hilo la kifamilia linaonesha wazi kuwa walioko karibu zaidi na Lissu wanataka suluhu ya haki na amani, tofauti na msukumo wa kisiasa unaoonekana kuendelezwa na baadhi ya viongozi na wanaharakati.
“Dada yake Lissu anaomba aachiwe kwa maridhiano. Hii ni sauti ya familia, ni sauti ya utu, lakini sauti hiyo inapuuzwa kwa sababu haileti faida ya kisiasa na kifedha kwa baadhi ya watu,” alisisitiza.
Mchange ameonyesha kuwa hivi sasa kuna mtifuano mkubwa baina ya viongozi wa CHADEMA ikiwemo Heche kutokuongea lugha moja na Lema, Sugu, Boni yai na wengine wanaodaiwa kumlalamikia Heche kujinufaisha
Akiendelea, Mchange amekosoa kile alichokiita unafiki wa kisiasa akirejea tukio la John Heche alipokamatwa. Amesema wakati huo familia ya Heche akiwemo mama yake walilia na kuomba msaada ili aachiwe, na hawakuiachia CHADEMA peke yake, bali waliomba msaada kwa pande mbalimbali.
“Heche alipokamatwa, mama yake alilia, ndugu zake waliomba msaada aachiwe.
Hakuna aliyesema aozee jela. Leo hii wanatoa msimamo mkali wa chama kana kwamba kufungwa ni ushindi wa kisiasa kwa Lissu,” amehoji.
Kutokana na mwenendo huo, Mchange aliomba Mahakama ichukue hatua kali za kisheria dhidi ya John Heche, akidai kuwa anaendelea kuitumia Mahakama kama jukwaa la siasa na chombo cha kupotosha umma kuhusu shauri linaloendelea.
“Mahakama inapaswa kulindwa. Iwapo kuna kiongozi anaitumia kupotosha umma na kushinikiza mwenendo wa kesi, basi achukuliwe hatua kali za kisheria ili kulinda heshima na uhuru wa mhimili huu,” alisema.
Amehitimisha kwa kutoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wanaharakati kuheshimu mipaka ya kisheria, kuacha siasa za kushangilia mateso ya wenzao, na kuweka mbele utu, maridhiano na amani ya taifa.
